HABARI NJEMA.... RUFAA YA BABU SEA NA MWANAWE KUSIKILIZWA MARCH MWAKA HUU

>


Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika (AfCHPR) katika kikao chake kilichoanza jijini Arusha, itapitia maombi ya rufani ya mwanamuziki maarufu nchini, Nguza Viking na John Viking dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na mahakama hiyo jana, ilieleza kuwa kesi hiyo namba 006/2015 iliyopangwa kusikilizwa Machi 11 haitasikilizwa katika mahakama ya wazi. 

Ni kesi mbili pekee kati ya 50 zitakazosikilizwa kwenye mahakama ya wazi, ikiwamo inayomhusu mwanasiasa maarufu wa Rwanda, Victoire Ingabire aliyoifungua kupinga ukiukwaji wa haki anaofanyiwa na Serikali yake. 

Pia, mahakama ilieleza kuwa kikao hicho cha 40 cha kawaida kitakamilika Machi 18 na kutoa uamuzi wa mashauri manne. 

Kesi ya Ingabire inayotarajiwa kuvuta hisia za watu wengi ikizingatiwa upinzani ambao amekuwa akiuonyesha dhidi ya serikali yake, itasikilizwa Machi 4. 

Katika kesi hiyo, Ingabire pamoja na mambo mengine anadai haki zake kuvunjwa ambazo zinatajwa kwenye Mkataba wa Mahakama hiyo Ibara ya 7, 10 na 18 hivyo anaitaka itoe uamuzi. 

Pia, Taasisi ya Action Pour la Protection des Droits de I’Homme (APDH) inaishtaki Serikali ya Ivory Coast kuvunja mkataba wa Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu Ibara ya 3 na 17 katika kesi namba 001/2014, iliyopangwa kusikilizwa Machi 3. 

Mahakama hiyo inaundwa na majaji 11 kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) na inakuwa na vikao vinne kwa mwaka, kufikia Januari 31 tayari ilikuwa imepokea kesi 74 kati ya hizo 25 imetolewa uamuzi. 

Maombi manne yamepelekwa  kwa uamuzi zaidi kwenye Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu.

>


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »