Ajifungulia kwenye beseni, nesi adundwa
MUUNGWANA BLOG / 2 hours ago
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo
SUZAN Anatory aliyeenda kujifungua katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana-Butimba na watoto wake wawili kufariki, kumesababisha Mariam Mkankule, nesi wa hospitali hiyo kudundwa.
Hatua hiyo iliibua vurugu na kusababisha Jeshi la Polisi Jijini Mwanza kuingilia kati kwa kutumia mabomu ya machozi kutuliza fujo hizo.
Tukio hilo limetokea leo katika hospitali hiyo baada ya muuguzi, Mariam kudaiwa kukataa kumpatia huduma mama huyo mjamzito.
Inaelezwa kuwa, chanzo kikubwa cha kutokea kwa vurugu hizo ni baada ya muuguzi huyo kumtolea lugha chafu na za vitisho mgonjwa huyo kitendo ambacho kiliibua hasira kwa wagonjwa wengine.
Pia inaelezwa kuwa, wakati muuguzi huyo akiendelea kutoa lugha hizo, Suzan alihisi maumivu na kwenda msalani ambako alijifungulia kwenye beseni watoto mapacha wawili ambao walikufa papo hapo.
Inadaiwa kuwa, baada ya wagonjwa kuona hali hiyo walianza kufanya vurugu muuguzi huyo, kabla ya polisi kufika na kupiga mabomu ya machozi na hatimaye kumwokoa muuguzi huyo.
Hata hivyo, Mariam na wenzake watano wanashikiliwa na polisi mjini hapa kwa mahojiano zaidi juu ya tukio hilo.
Baadhi ya wagonjwa waliokuwepo katika hospitali hiyo na kushuhudia wamesema kuwa, muuguzi huyo alikuwa akiwaambia haogopi chochote.
Taabu Abdallah amesema, “mimi nilikuwepo hapa na niliona kila kitu, yule mjamzito alifika hapa kwa lengo la kujifungua na akamueleza muuguzi muda wake umefika lakini alikataa kumhudumia.”
Amesema, wakati wakivutana huku muuguzi huyo akidai kwamba haogopi chochote na hawezi kumhudumia mama huyo.
Suzan amesema kuwa, msaada kukosa kutoka kwa wauguzi ndio chanzo kilichosababisha kufa kwa watoto wake.
Amesema, sababu zilizokuwa zikitolewa na muuguzi huyo kwamba siku zake za kujifungua hazijafika sio kweli.
“Mimi baada ya kuvutana na huyo muuguzi, nilikwenda msalani baada ya kujisikia vibaya nikiwa najisaidia haja ndogo ghafla nilijifungua mtoto wa kwanza ambaye alikuwa ametanguliza makalio.
“Pia mtoto wa pili nilijifungua akiwa mzima lakini msaada kutoka kwa wauguzi ndio ulisababisha huyu mtoto akafariki na kama angepata msaada asingefariki,” amesema Suzan.
Magesa Mulongo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amesema tume imeundwa kuchunguza suala hilo na kwamba hatua zitachukuwa juu yake pamoja na wenzake pale itakapobainika kuhusika kwao.
“Muda huu tume hii iliyoundwa wakati ikiendelea kuchunguza suala hili, hatua zaidi zitaendelea kuchukuliwa,” amesema Mulongo.
Hata hivyo, Mulongo aliwasimamisha kazi madaktari Ngusa Masanja, Vivian Moshi na Mariam kwa uchunguzi zaidi