Moshi/Arusha. Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, wameamuru kurudiwa kusikilizwa kwa kesi ya mauaji ya askari polisi mwaka 2007 akiwa lindo katika Benki ya NMB, Tawi la Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Pia, wamefuta mwenendo wa kesi iliyowatia hatiani raia wawili wa Kenya na Mtanzania mmoja waliohukumiwa adhabu ya kifo.
Adhabu hiyo ya kifo ilitolewa Juni 11,2014 na Jaji Kakusulo Sambo dhidi ya raia wa Kenya, Samwel Gitau Saitoti na Michael Kimani na kumhukumu Mtanzania, Calist Kanje kifungo cha miaka mitano.
Kanje ambaye ni mfanyabiashara anayemiliki vitega uchumi kadhaa vikiwamo vituo vya mafuta na mashamba, alipatikana na hatia ya kuwasaidia raia hao wa Kenya baada ya mauaji.
Polisi huyo wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Michael Milanzi, aliuawa kwa kupigwa risasi Julai 11, 2007, baada ya majambazi kuvamia benki hiyo na kupora Sh239 milioni.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa kutakuwa na changamoto itakayoukabili upande wa mashtaka ya kuanza kukusanya upya mashahidi zaidi ya 50 wa kesi hiyo.
Uamuzi wa kusikilizwa kesi hiyo upya ulitolewa juzi na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, Mbarouk Salum, Benard Luanda na Mussa Kipenga katika kikao kilichoketi jijini Arusha.
Majaji hao walisema wamebaini katika mwenendo wa kesi hiyo iliyosikilizwa Moshi, wazee washauri wa mahakama hawakupewa nafasi inayostahili ili kuiwezesha mahakama kufikia uamuzi sahihi.
Walisema katika shauri hilo, wamebaini makosa kadhaa ya kisheria na hivyo, wameagiza kufutwa mwenendo wote wa kesi na ianze upya baada ya washtakiwa wote watatu kukata rufaa.
Licha ya Kanje aliyekuwa amejiondoa katika rufaa hiyo siku chache kabla ya kuanza kusikilizwa kwa rufaa hiyo, majaji hao walisema usikilizwaji huo utamuhusisha.
“Tunaamuru kesi ya warufani isikilizwe upya mbele ya Jaji mwingine na wazee washauri wengine wa mahakama katika muda mfupi kadiri iwezekanavyo,” alisema Jaji Salum kwa niaba ya wenzake.
Awali, wakili John Materu anayewatetea washitakiwa hao, alidai mwenendo wa kesi ulikuwa na dosari za kisheria kwa vile mchango wa wazee washauri wa mahakama hauonekani kwenye kumbukumbu.
Mawakili waandamizi wa Serikali, Hassan Nkya na Stella Majaliwa, walikubaliana na hoja ya wakili Materu kuhusiana na dosari hizo ambazo ziliifanya mahakama kufikia uamuzi.
Raia hao wa Kenya waliopambana na polisi jijini Arusha kwa saa sita mfululizo mwaka 2007, pia wanatumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kupora Sh239 milioni mali ya NMB.