Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, CP Simon Sirro (pichani) amesema kuwa jeshi lake linafuatilia kwa karibu madai mawili, kwamba kuna watu wanajipati mamilioni ya shilingi kwa kuuza fomu wanazodai ni za kujiunga na taasisi maarufu duniani ya Freemaso
Pili kuwepo kwa madai kwamba eti watu wanaojiunga na taasisi hiyo wamekuwa wakitoa makafara watu wao wa karibu kama moja ya masharti ya kujiunga, Uwazi lina habari yote.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jijini Dar hivi karibuni, Kamanda Sirro alisema kufuatia malalamiko hayo, amemwagiza Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ZCO Masawe kupeleka makachero kwenye jengo hilo ili kufanya uchunguzi wa kina wa kuwabaini wahusika na kuwanasa mpaka kwenye vyombo vya sheria.
Alama za Freemason.
“Nimewasikia kuhusu hao watu wanaowatapeli wananchi wakijifanya wanauza fomu ya kujiunga na Freemason, pia kama kweli kuna wanaojiunga wakiwatoa kafara watu, nimeshamwagiza ZCO Masawe apange timu aende kwenye eneo hilo ili kuwanasa watu wao.
“Watanzania wenyewe pia wanatakiwa kuwa makini sana na watu wa aina hiyo kwani kama mtu anataka kukutapeli anajulikana tu,” alisema Kamanda Sirro.
POLISI WAMEANZA
Taarifa zaidi kutoka ndani ya jeshi hilo zinadai kuwa, tayari polisi wameshafika eneo husika na kufanya uchunguzi wao na wanaendelea nao.
“Agizo la afande Sirro tayari polisi wanalifanyia kazi, wakati wowote ule utasikia watu wamekamatwa maana tumepewa ushirikiano mkubwa na walinzi wa eneo lile,” alisema mtoa taarifa mmoja ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe kwa sababu yeye si msemaji wa jeshi hilo.
WALINZI FREEMASON WAZUNGUMZA
walinzi walikiri kuwepo kwa watu wanaosimama jirani kabisa na geti la kuingia ndani ya jengo hilo wakisema wanauza fomu za kujiunga na taasisi hiyo.
Lakini wakakanusha habari kwamba kuna wanaojiunga kwa kutoa kafara ndugu zao wakisema ni maneno ya mitaani ambayo yameenea duniani kote.
John Ngonyani ni mlinzi wa eneo hilo ambaye alisema Ofisi za Freemason zilifungwa tangu Novemba 15, mwaka jana na viongozi wote wapo likizo hadi Machi 15, mwaka huu.
“Siyo hapa tu kumefungwa bali hata ofisi zilizopo mikoani yaani Arusha, Mbeya, Mwanza na Kilimanjaro nazo zimefungwa hadi Machi 15,” alisema mlinzi huyo.
Alisema: “Kwamba sasa shughuli zote za kiofisi hapa zimesitishwa hadi hapo viongozi watakaporudi, Machi 15. Hamna mambo ya kafara, hayo ni maneno ya watu mitaani tu. Hii ni taasisi ya kusaidia jamii, ipo duniani kote.”
Mlinzi huyo alisema, Jumatatu hadi Ijumaa ndiyo watu wengi wanaotaka kujiunga hufika hapo lakini Jumamosi na Jumapili ni wachache huku akisisitiza kuwa, hakuna mambo ya kafara zaidi ya watu kusaidiana.
ILIWAHI KUANDIKWA
Hivi karibuni kikosi cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) cha Global Publishers kilipokea malalamiko kutoka kwa watu ‘waliopigwa’ kutokana na tamaa ya utajiri kwa kuuziwa fomu feki za kujiunga na Freemason.
Baada ya malalamiko kutoka, OFM waliingia mzigoni kuchunguza ili kubaini ukweli wa malalamiko hayo na kuandikwa na gazeti ndugu na hili, Amani linalotoka kila Alhamisi.
Makamanda wa OFM walifunga safari hadi kwenye jengo hilo na kumfuatilia kila mmoja aliyekuwa akipita ambapo waliweza kugundua kuwepo kwa jambo hilo lakini kwa siri.
Kamanda mmoja wa OFM alishika bahasha yenye fomu ndani na kuweka maelezo kuwa ni za Freemason ambapo katika watu watano waliopita eneo hilo, wanne walitaka kununua kwa kuulizia bei. Wengine walifika na kuuliza jinsi ya kuingia kwenye ofisi hizo ili wakapewe maelekezo ya kujiunga.
Mlinzi mmoja wa jengo hilo alishangaa Watanzania wanaokubali kuuziwa fomu nje ya jengo hilo.
“Mimi nawashangaa sana Watanzania. Kama kweli kuna fomu kwa nini mtu akuuzie nje. Viongozi wenyewe wakishaingia ndani hatujui wanachofanya. Kama ni fomu si tungekuwa tunaona watu wakiingia na kutoka nazo,” alisema mlinzi mmoja.